“Elimu bahari haiishi kwa kuchotwa”anasema Kibibi Hillary mwanafunzi na mjasiriamali mdogo. Elimu anayopata katika kozi ya uhandisi wa kiraia katika chuo kikuu cha Makerere sio tu elimu ya mafunzo ya darasani pekee bali pia ya utunzaji wa mazingira katika jamii.
Kwa muda mrefu wa kuishi nchini Uganda huku akiendelea na masomo yake, Kibibi aliamua kulivali njuga suala la uchafuzi wa mazingira hasa katika mji mkuu Kampala ambapo mifuko ya plastiki maarufu kwa wenyeji kama “kaveera” hutumiwa zaidi na Waganda. Wengi kwa ununuzi wa mboga, nguo na mahitaji mengine ya kila siku kwa sababu mifuko hiyo ni ya bei nafuu na rahisi kupatikana. Ijapokuwa ni rahisi kupatikana na inarahisisha shughuli za ununuzi wa bidhaa kadha wa kadha mifuko ya ya plastiki husababisha gharama kubwa sana katika utunzaji wa mazingira nchini Uganda.
Mifuko hiyo huchafua mazingira kwani inapotupwa kwenye udongo kiholela, inatoa kemikali zenye sumu ambayo wanyama hula na mara nyingi hupoteza maisha yao. Kadalika ina madhara makubwa kwa uhai wa viumbe hai wa majini.
Licha ya madhara yake, takwimu za mwaka 2008 za Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMA) zinaonyesha kuwa raia wa Uganda hutumia tani 25,900 za mifuko ya plastiki kila mwezi. Tani mia tisa ambayo ni sawa na 20% ya mifuko hiyo huzalishwa na viwanda 15 wakati tani 25,000 sawia na 80% zinaingizwa nchini kila mwezi.
Kulingana na takwimu hizo, Kampala inazalisha zaidi ya tani 350,000 za taka ngumu kila mwaka na ni nusu tu ya takataka hiyo inayokusanywa na kuacha mifuko hiyo kwenye mifereji ambayo husababisha kuziba kwa mifereji na kusababisha mafuriko makubwa.
Baada ya kutafiti kuhusu athari za utumiaji wa mifuko ya plastiki, Kibibi aliamua kujifunza na kuanza kutengeneza mifuko ya karatasi kama mojawapo ya njia ya kukomesha uharibu wa mazingira nchini Uganda.
Tayari mataifa jirani ikiwemo Rwanda, Kenya na Tanzania yamepiga marufuku utumiaji na uuzaji wa mifuko ya plastiki.
Kupitia pesa ya matumizi aliyokuwa akitumiwa na wazazi, kibibi alitoa shillingi elfu hamsini za Uganda na kununua mahitaji mbalimbali kama karatasi na kamba za kushikilia mifuko.
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa kampuni yake anayoiita Makhia Enterprises Limited, ambayo ilifunguliwa rasmi mwaka jana 2021 mwezi wa 3 na inayojishughulisha na utengenezaji wa mifuko ya makaratasi. Katika hiyo mifuko ya karatasi anaweka nembo yoyote mteja anayotaka iwe ya rangi au hisiyo ya rangi. Pia mifuko yake inaweza kutumika zaidi ya mara tatu katika kutunza bidhaa yoyote za kutoka sokoni, madukani nakadhalika.
Mwanzo wa biashara yoyote huwa ni mgumu, kwani wateja walikuwa ni wachache sana na ndio ilikuwa changamoto kubwa kwake ila hakukata tamaa bali alitumia mbinu zingine kama utumiaji wa mitandao ya kijamii kama Facebook, Instragram na Whatsapp kutangaza biashara yake.
Hakika mbinu hiyo ilileta matumaini na hatimaye alianza kupata wateja kwa wingi kutoka makapuni binafsi na watu binafsi. Makhia Enterprises Limited, hadi sasa inaweza kutengeneza mifuko 700 na zaidi.
Ama kweli Hillary ni mfano mzuri wa kuigwa na vijana, kama unakipaji chochote usikikalie kwa sababu, hakuna mtu atakayekufahamu au ulimwengu kukutambua. Ni lazima utumie kipaji kujiendeleza katika maisha.